2 Nya. 9:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.

2. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie.

3. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,

4. na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA; roho yake ilizimia.

5. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.

6. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.

7. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.

8. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake BWANA, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.

9. Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.

10. Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani.

2 Nya. 9