2 Nya. 6:6-18 Swahili Union Version (SUV)

6. lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli.

7. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.

8. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako;

9. lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu.

10. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.

11. Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la BWANA, alilolifanya na wana wa Israeli.

12. Akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono;

13. (maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake mikono mitano, na upana wake mikono mitano, na kwenda juu kwake mikono mitatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni);

14. akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote;

15. uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.

16. Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu.

17. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi.

18. Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga!

2 Nya. 6