12. Wakaziondoa sadaka za kuteketezwa, wawape wana wa watu, kama walivyogawanyika kufuata nyumba za mababa, ili wamtolee BWANA, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Musa. Nao ng’ombe wakawafanya vivyo hivyo.
13. Wakaioka moto pasaka kama ilivyo sheria; wakatokosa matoleo matakatifu vyunguni, na masufuriani, na makaangoni, wakawachukulia upesi wana wa watu wote.
14. Baadaye wakajiandalia wenyewe, na makuhani; kwa sababu makuhani, wana wa Haruni, walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta hata usiku; kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe, na makuhani, wana wa Haruni.
15. Nao waimbaji, wana wa Asafu wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia.
16. Basi huduma yote ya BWANA ikatengenezwa siku ile ile, kuifanya pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya BWANA, kama alivyoamuru mfalme Yosia.
17. Wana wa Israeli waliokuwapo wakafanya pasaka wakati ule, na sikukuu ya mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
18. Wala haikufanyika pasaka kama ile katika Israeli tangu siku za nabii Samweli; wala wafalme wa Israeli hawakufanya hata mmoja wao pasaka kama ile Yosia aliyoifanya, pamoja na makuhani, na Walawi, na Yuda wote na Israeli waliokuwapo, na wenyeji wa Yerusalemu.
19. Katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Yosia ikafanyika pasaka hiyo.
20. Baada ya hayo yote, alipokwisha Yosia kulitengeneza hekalu, Neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana Karkemishi karibu na Frati; naye Yosia akatoka juu yake.
21. Lakini yeye akatuma kwake wajumbe, kusema, Ni nini niliyo nayo mimi na wewe, Ee mfalme wa Yuda? Sikuja juu yako leo, lakini juu ya nyumba niliyo na vita nayo; naye Mungu ameniamuru nifanye haraka; acha basi kumpinga Mungu, aliye pamoja nami, asikuharibu.
22. Walakini Yosia hakukubali kumgeuzia uso mbali, akajibadilisha apate kupigana naye, asiyasikilize maneno ya Neko, yaliyotoka kinywani kwa Mungu, akaja kupigana bondeni mwa Megido.