27. kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema BWANA.
28. Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari.
29. Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.
30. Akapanda mfalme nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, na makuhani na Walawi, na watu wote, wakubwa kwa wadogo; naye akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana nyumbani mwa BWANA.
31. Akasimama mfalme mahali pake, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuzishika amri zake, na shuhuda zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, kuyatenda maneno ya agano yaliyoandikwa kitabuni humo.
32. Akawafanya wote walioonekana katika Yerusalemu na Benyamini walikubali. Na wenyeji wa Yerusalemu wakafanya sawasawa na agano la Mungu, Mungu wa baba zao.
33. Naye Yosia akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi zote zilizokuwa milki ya wana wa Israeli, akawafanya wote walioonekana katika Israeli kutumika, naam, wamtumikie BWANA, Mungu wao. Siku zake zote hawakuacha kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.