2 Nya. 34:23-31 Swahili Union Version (SUV)

23. Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu,

24. BWANA asema hivi, Angalia, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, laana zote zilizoandikwa katika kitabu hicho walichokisoma mbele ya mfalme wa Yuda;

25. kwa sababu wameniacha mimi, na kuifukizia uvumba miungu mingine, ili wanikasirishe mimi kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo ghadhabu yangu imemwagika juu ya mahali hapa, wala isizimike.

26. Lakini mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kwa habari ya maneno uliyoyasikia,

27. kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema BWANA.

28. Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari.

29. Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.

30. Akapanda mfalme nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, na makuhani na Walawi, na watu wote, wakubwa kwa wadogo; naye akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana nyumbani mwa BWANA.

31. Akasimama mfalme mahali pake, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuzishika amri zake, na shuhuda zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, kuyatenda maneno ya agano yaliyoandikwa kitabuni humo.

2 Nya. 34