9. Lakini kulikuwako huko nabii wa BWANA, jina lake aliitwa Odedi; akatoka kuwalaki jeshi waliokuja Samaria, akawaambia, Angalieni, kwa kuwa BWANA, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, yeye amewatia mikononi mwenu, nanyi mmewaua kwa ghadhabu iliyofikia mbinguni.
10. Na sasa mwanuia kuwatawala wana wa Yuda na Yerusalemu, wawe kwenu watumwa na wajakazi; lakini ninyi nanyi je! Hamna hatia zenu wenyewe juu ya BWANA, Mungu wenu?
11. Haya, nisikieni mimi basi, mwarudishe wafungwa, mliowachukua mateka wa ndugu zenu; kwa maana ghadhabu ya BWANA iliyo kali i juu yenu.
12. Ndipo wakaondoka juu ya hao waliotoka vitani baadhi ya wakuu wa wana wa Efraimu, Azaria, mwana wa Yohanani, na Berekia mwana wa Meshilemothi, na Yehizkia mwana wa Shalumu, na Amasa mwana wa Hadlai,
13. wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za BWANA, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli.
14. Basi watu wenye silaha wakawaacha wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote.
15. Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wote wao waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria.
16. Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie.
17. Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.
18. Wafilisti pia walikuwa wameingia miji ya Shefela, na ya Negebu ya Yuda, nao wameutwaa Beth-shemeshi, na Ayaloni, na Gederothi, na Soko pamoja na miji yake, na Timna pamoja na miji yake, na Gimzo pia na miji yake; wakakaa humo.
19. Kwa maana BWANA aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi BWANA mno.