19. Kwa maana BWANA aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi BWANA mno.
20. Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lo lote.
21. Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya BWANA, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo.
22. Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi BWANA, huyo mfalme Ahazi.
23. Kwani akaitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.
24. Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya BWANA; akajifanyizia madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu.
25. Na katika kila mji wa Yuda akafanya mahali pa juu pa kuifukizia miungu mingine uvumba, akamkasirisha BWANA, Mungu wa babaze.
26. Basi mambo yake yote yaliyosalia, na njia zake zote, za kwanza na za mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
27. Ahazi akalala na babaze, wakamzika mjini, yaani, Yerusalemu; maana hawakumleta makaburini mwa wafalme wa Israeli; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.