13. wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za BWANA, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli.
14. Basi watu wenye silaha wakawaacha wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote.
15. Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wote wao waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria.
16. Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie.
17. Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.
18. Wafilisti pia walikuwa wameingia miji ya Shefela, na ya Negebu ya Yuda, nao wameutwaa Beth-shemeshi, na Ayaloni, na Gederothi, na Soko pamoja na miji yake, na Timna pamoja na miji yake, na Gimzo pia na miji yake; wakakaa humo.
19. Kwa maana BWANA aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi BWANA mno.
20. Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lo lote.
21. Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya BWANA, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo.
22. Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi BWANA, huyo mfalme Ahazi.
23. Kwani akaitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.
24. Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya BWANA; akajifanyizia madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu.