15. Akafanya katika Yerusalemu mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu wastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kutupa mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.
16. Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi BWANA, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa BWANA, ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia.
17. Azaria kuhani akaingia nyuma yake, na pamoja naye makuhani themanini wa BWANA, mashujaa;
18. wakamzuia Uzia mfalme, wakamwambia, Si haki yako, Uzia, kumfukizia BWANA uvumba, ila ni haki ya makuhani wana wa Haruni, waliofanywa wakfu, ili wafukize uvumba; toka katika patakatifu; kwa kuwa umekosa; wala haitakuwa kwa heshima yako kutoka kwa BWANA, Mungu.
19. Akaghadhibika Uzia; naye alikuwa na chetezo mkononi cha kufukizia uvumba; naye hapo alipowaghadhibikia makuhani, ukamtokea ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa BWANA karibu na madhabahu ya kufukizia.
20. Azaria kuhani mkuu na makuhani wote wakamtazama, na angalia, alikuwa na ukoma pajini mwa uso, wakamtoa humo upesi; hata na yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa sababu BWANA amempiga.
21. Uzia mfalme akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee, kwa kuwa ni mwenye ukoma; maana alitengwa na nyumba ya BWANA; na Yothamu mwanawe alikuwa juu ya nyumba ya mfalme, akiwahukumu watu wa nchi.
22. Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, aliyaandika Isaya nabii, mwana wa Amozi.
23. Basi Uzia akalala na babaze; wakamzika pamoja na babaze katika konde la kuzikia la wafalme; kwa kuwa walisema, Huyu ni mwenye ukoma. Na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake.