2 Nya. 26:12-19 Swahili Union Version (SUV)

12. Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita.

13. Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, mia tatu na saba elfu, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui.

14. Uzia akawafanyizia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo.

15. Akafanya katika Yerusalemu mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu wastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kutupa mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.

16. Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi BWANA, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa BWANA, ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia.

17. Azaria kuhani akaingia nyuma yake, na pamoja naye makuhani themanini wa BWANA, mashujaa;

18. wakamzuia Uzia mfalme, wakamwambia, Si haki yako, Uzia, kumfukizia BWANA uvumba, ila ni haki ya makuhani wana wa Haruni, waliofanywa wakfu, ili wafukize uvumba; toka katika patakatifu; kwa kuwa umekosa; wala haitakuwa kwa heshima yako kutoka kwa BWANA, Mungu.

19. Akaghadhibika Uzia; naye alikuwa na chetezo mkononi cha kufukizia uvumba; naye hapo alipowaghadhibikia makuhani, ukamtokea ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa BWANA karibu na madhabahu ya kufukizia.

2 Nya. 26