11. Zaidi ya hayo Uzia alikuwa na jeshi la watu wa kupigana, waliokwenda vitani vikosi vikosi, sawasawa na hesabu walivyohesabiwa na Yeieli mwandishi, na Maaseya msimamizi, chini ya mkono wa Hanania, mmojawapo wa maakida wa mfalme.
12. Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita.
13. Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, mia tatu na saba elfu, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui.
14. Uzia akawafanyizia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo.
15. Akafanya katika Yerusalemu mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu wastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kutupa mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.