1. Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, naye alikuwa mwenye miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa Amazia babaye.
2. Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.
3. Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.
4. Akafanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye.
5. Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta BWANA, Mungu alimfanikisha.
6. Akatoka akapigana na Wafilisti, akauvunja ukuta wa Gathi, na ukuta wa Yabne, na ukuta wa Ashdodi; akajenga miji katika Ashdodi na katikati ya Wafilisti.
7. Mungu akamsaidia juu ya Wafilisti, na juu ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na juu ya Wameuni.