7. Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya BWANA wamewapatia mabaali.
8. Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya BWANA.
9. Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea BWANA kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani.
10. Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha.
11. Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele.
12. Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya BWANA; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya BWANA, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya BWANA.
13. Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara.
14. Nao walipokwisha, wakaleta mbele ya mfalme na Yehoyada fedha iliyobaki, vikafanyizwa kwayo vyombo vya nyumba ya BWANA, vyombo vya utumishi, navyo vya kutolea, na miiko, na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya BWANA, daima, siku zote za Yehoyada.
15. Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye umri mwingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia na thelathini.
16. Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.
17. Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.
18. Wakaiacha nyumba ya BWANA, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.
19. Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa BWANA; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.