1. Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Sibia wa Beer-sheba.
2. Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA siku zote za Yehoyada kuhani.
3. Yehoyada akamwoza wake wawili, naye akazaa wana na binti.
4. Ikawa baada ya haya, Yoashi alikuwa na nia ya kuitengeneza nyumba ya Mungu.
5. Akawakusanya makuhani na Walawi, akawaambia, Nendeni mijini mwa Yuda, mkakusanye katika Israeli wote fedha, ili kuitengeneza nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka, mkafanye bidii kuliharakisha neno hili. Walakini Walawi hawakuliharakisha.
6. Mfalme akamwita Yehoyada mkuu wao, akamwambia, Mbona hukuwataka Walawi waitoze Yuda na Yerusalemu kodi ya Musa mtumishi wa BWANA, na ya kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya hema ya ushuhuda?
7. Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya BWANA wamewapatia mabaali.
8. Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya BWANA.