4. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA.
5. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa BWANA, mbele ya ua mpya;
6. akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako.
7. Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele?
8. Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema,
9. Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa.
10. Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu;
11. tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha.
12. Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako.
13. Wakasimama Yuda wote mbele za BWANA, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao.
14. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko;
15. akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.
16. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli.