13. Wakasimama Yuda wote mbele za BWANA, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao.
14. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko;
15. akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.
16. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli.
17. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yu pamoja nanyi.
18. Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za BWANA Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia BWANA.
19. Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.
20. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.
21. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele.
22. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa.
23. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe.