1. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake, akajitia nguvu juu ya Israeli.
2. Akaweka jeshi katika miji yote yenye maboma ya Yuda, akatia na askari walinzi katika nchi ya Yuda, na katika miji ya Efraimu, aliyoitwaa Asa babaye.
3. Naye BWANA alikuwa pamoja na Yehoshafati, kwa kuwa alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute mabaali;
4. lakini alimtafuta Mungu wa baba yake, akaenda katika amri zake, wala si katika matendo ya Israeli.
5. Kwa hiyo BWANA akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na Yuda wote; basi akawa na mali na heshima tele.
6. Ukainuliwa moyo wake katika njia za BWANA; na zaidi ya hayo akapaondoa mahali pa juu, na maashera, katika Yuda.
7. Tena, katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake, akawatuma wakuu wake, yaani, Ben-haili, na Obadia, na Zekaria, na Nethaneli, na Mikaya, ili kufundisha mijini mwa Yuda;
8. na pamoja nao Walawi, yaani, Shemaya, na Nethania, na Zebadia, na Asaheli, na Shemiramothi, na Yehonathani, na Adonia, na Tobia, na Tob-adonia, Walawi; na pamoja nao Elishama na Yehoramu, makuhani.
9. Wakafundisha katika Yuda, wenye kitabu cha torati ya BWANA; wakazunguka katika miji yote ya Yuda, wakafundisha kati ya watu.