2 Nya. 15:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;

2. naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.

3. Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;

4. lakini walipomgeukia BWANA, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.

5. Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.

6. Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.

7. Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.

8. Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaifanyiza tena madhabahu ya BWANA, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa BWANA.

9. Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimwangukia wengi katika Israeli, walipoona kwamba BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.

10. Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.

2 Nya. 15