5. Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanyiza Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea.
6. Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake.
7. Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe.
8. Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake.
9. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi.
10. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi?
11. Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao;