7. Wala si kwa kuja kwake tu, bali kwa zile faraja nazo alizofarijiwa kwenu, akituarifu habari ya shauku yenu, na maombolezo yenu, na bidii yenu kwa ajili yangu, hata nikazidi kufurahi.
8. Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu.
9. Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote.
10. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.
11. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.
12. Basi, ijapokuwa naliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu.