3. Hakika kwa amri ya BWANA mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;
4. tena kwa ajili ya damu zisizo na hatia alizozimwaga; kwani aliujaza Yerusalemu damu zisizo na hatia; wala BWANA hakukubali kusamehe.
5. Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
6. Yehoyakimu akalala na babaze; na mwanawe Yekonia akatawala mahali pake.
7. Basi mfalme wa Misri hakuja tena kutoka nchi yake; kwa kuwa mfalme wa Babeli alikuwa amemnyang’anya nchi, tangu kijito cha Misri mpaka mto wa Frati, yote aliyokuwa nayo mfalme wa Misri.
8. Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu.
9. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake.
10. Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa.
11. Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru.
12. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.