1. Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu.
2. Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa BWANA, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya BWANA.
3. Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za BWANA, kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.