2 Fal. 17:1-13 Swahili Union Version (SUV)

1. Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kenda.

2. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia.

3. Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi.

4. Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni.

5. Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu.

6. Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi.

7. Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya BWANA, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine.

8. Wakaziendea sheria za mataifa, ambao BWANA aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya.

9. Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya BWANA, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.

10. Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;

11. wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao BWANA aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe BWANA;

12. wakatumikia sanamu, ambazo BWANA aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili.

13. Pamoja na hayo BWANA aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu.

2 Fal. 17