1 The. 2:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Maana ninyi wenyewe, ndugu, mwakujua kuingia kwetu kwenu, ya kwamba hakukuwa bure;

2. lakini tukiisha kuteswa kwanza na kutendwa jeuri, kama mjuavyo, katika Filipi, twalithubutu katika Mungu kuinena Injili ya Mungu kwenu, kwa kuishindania sana.

3. Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila;

4. bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu.

5. Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo, wala maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi.

6. Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo;

7. bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe.

8. Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.

9. Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu.

1 The. 2