16. Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia.
17. Hata Samweli alipomwona Sauli, BWANA akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.
18. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi?
19. Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako.
20. Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?