10. Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu.
11. Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?
12. Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu;
13. mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona.
14. Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu.
15. Basi BWANA alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema,
16. Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia.
17. Hata Samweli alipomwona Sauli, BWANA akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.