17. Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia.
18. Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili.
19. Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote.
20. Naye Daudi akatwaa makundi yote ya kondoo na ng’ombe, ambao waliwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine, wakasema, Hao ndio nyara za Daudi.
21. Kisha Daudi aliwafikilia wale watu mia mbili, waliokuwa wametaka kuzimia, hata wasiweze kumfuata Daudi, wale waliowaacha wakae karibu na kijito cha Besori; nao wakatoka nje ili kumlaki Daudi, na kuwalaki hao watu waliokuwa pamoja naye, naye Daudi alipowakaribia hao watu, aliwasalimu.
22. Ndipo watu waovu wote na wale wasiofaa, miongoni mwa hao waliokwenda pamoja na Daudi, wakasema, Kwa kuwa watu hawa hawakuenda pamoja na sisi, hatutawapa kitu cho chote katika hizo nyara tulizozitwaa tena, isipokuwa kila mtu atapewa mkewe na watoto wake, wawachukue na kwenda zao.