1. Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako.
2. Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinda kichwa changu daima.
3. Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Israeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi.
4. Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa.