29. Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na BWANA, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo.
30. Tena itakuwa, hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli;
31. hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo BWANA atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako.
32. Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki;
33. na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.
34. Kwa kuwa ni kweli, aishivyo BWANA, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.