1. Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
2. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.
3. Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu.
4. Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.
5. Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi.
6. Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka.
7. Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa maakida wa watu elfu, na maakida wa watu mia;
8. hata ninyi nyote mkafanya fitina juu yangu, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemwondokesha mtumishi wangu juu yangu, anivizie kama hivi leo?
9. Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nalimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu.
10. Naye akamwuliza BWANA kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti.