4. Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali.
5. Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni.
6. Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wa katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika.
7. Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa akaliko huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka.
8. Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye.
9. Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa.