21. Zekaria, mwana wa Meshelemia, alikuwa bawabu mlangoni pa ile hema ya kukutania.
22. Hao wote waliochaguliwa kuwa wangojezi wa malango walikuwa watu mia mbili na kumi na wawili. Nao wakahesabiwa kwa nasaba katika vijiji vyao, ambao Daudi na Samweli, huyo mwonaji, walikuwa wamewaweka katika kazi yao waliyoamaniwa.
23. Basi watu hao na wana wao walikuwa na usimamizi wa malango ya nyumba ya BWANA, yaani, nyumba ya maskani, kwa zamu.
24. Hao wangojezi walikuwapo pande zote nne, kuelekea mashariki, na magharibi, na kaskazini, na kusini.
25. Na ndugu zao, katika vijiji vyao, wakaamaniwa kuingia kila siku ya saba, zamu kwa zamu, ili kuwa pamoja nao;
26. kwa maana wale wangojezi wanne, waliokuwa wakuu, nao ni Walawi, walikuwa na kazi ya kuamaniwa, tena walikuwa juu ya vyumba na juu ya hazina katika nyumba ya Mungu.