1. Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na maakida wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, waume mashujaa wote.
2. Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nalikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kustarehe kwa ajili ya sanduku la agano la BWANA, na kiti cha kuwekea miguu yake cha Mungu wetu; hata nalikuwa nimeweka tayari kwa kujenga.
3. Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu.
4. Walakini BWANA, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote;
5. tena katika wana wangu wote (kwani BWANA amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa BWANA, juu ya Israeli.
6. Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye.
7. Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo.
8. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la BWANA, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za BWANA, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele.