1 Nya. 26:10-19 Swahili Union Version (SUV)

10. Hosa naye, wa wana wa Merari, alikuwa na wana; Shimri mkuu wao; (kwani ajapokuwa yeye si mzaliwa wa kwanza, babaye alimweka mkuu);

11. Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu, Zekaria wa nne; wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa watu kumi na watatu.

12. Katika hao zilikuwa zamu za mabawabu, yaani, katika hao wakuu, wenye ulinzi sawasawa na ndugu zao, wa kutumika katika nyumba ya BWANA.

13. Nao wakatupiwa kura kwa ajili ya kila lango, wadogo sawasawa na wakubwa, kwa kadiri ya mbari za baba zao.

14. Kura ya mashariki ya lango ikamwangukia Meshelemia. Ndipo wakamtupia kura Zekaria mwanawe, mshauri mwenye busara; na kura yake ikamtokea ya kaskazini.

15. Ya Obed-edomu ya kusini; na ya wanawe nyumba ya akiba.

16. Ya Shupimu na Hosa upande wa magharibi, langoni pa Shalekethi, hapo penye daraja ya kupandia, ulinzi kwa ulinzi.

17. Upande wa mashariki walikuwapo Walawi sita, kaskazini wanne kila siku, kusini wanne kila siku, na wa nyumba ya akiba wawili wawili.

18. Penye Parbari upande wa magharibi, walikuwapo wanne darajani, na wawili huko Parbari.

19. Hizo ndizo zamu za mabawabu; wa wana wa Wakora, na wa wana wa Merari.

1 Nya. 26