1 Nya. 22:4-15 Swahili Union Version (SUV)

4. na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro wakamletea Daudi mierezi tele.

5. Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.

6. Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba.

7. Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu.

8. Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu;

9. tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake;

10. huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakifanya imara milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli.

11. Sasa mwanangu, BWANA na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA, Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako.

12. BWANA na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike torati ya BWANA, Mungu wako.

13. Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu, BWANA alizomwagizia Musa juu ya Israeli; uwe hodari, na wa moyo mkuu; usiogope wala usifadhaike.

14. Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya BWANA, talanta elfu mia za dhahabu, na talanta elfu elfu za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza.

15. Tena kwako kuna mafundi wengi, wenye kuchonga na kufanyiza kazi ya mawe na miti, na kila aliye mstadi kwa kazi yo yote;

1 Nya. 22