2. Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu.
3. Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyo na uzani;
4. na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro wakamletea Daudi mierezi tele.
5. Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.
6. Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba.
7. Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu.
8. Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu;
9. tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake;
10. huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakifanya imara milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli.