1 Nya. 17:7-14 Swahili Union Version (SUV)

7. Basi sasa ndivyo utakavyomwambia mtumishi wangu Daudi, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli;

8. nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina, kama jina la hao wakuu walioko duniani.

9. Tena nitawaagizia watu wangu Israeli mahali, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena kama hapo kwanza,

10. na tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi wawe juu ya watu wangu Israeli, nami nitawashinda adui zako wote. Pamoja na hayo nakuambia, ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.

11. Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake.

12. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele.

13. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako;

14. ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.

1 Nya. 17