1. Basi Wafilisti wakapigana juu ya Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima Gilboa.
2. Nao Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe; Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli.
3. Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde.
4. Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao, wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.
5. Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa.
6. Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu; na nyumba yake yote wakafa pamoja.