8. Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi!
9. Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu.
10. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima.
11. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao;
12. kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili;
13. tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa.
14. Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali kuwaonya kama watoto niwapendao.
15. Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
16. Basi, nawasihi mnifuate mimi.
17. Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.
18. Basi wengine wamejivuna kana kwamba siji kwenu.
19. Lakini nitakuja kwenu upesi, nikijaliwa, nami nitafahamu, si neno lao tu waliojivuna, bali nguvu zao.
20. Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno, bali katika nguvu.
21. Mnataka vipi? Nije kwenu na fimbo, au nije katika upendo na roho ya upole?