44. hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.
45. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.
46. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.
47. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.
48. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.
49. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.
50. Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.
51. Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52. kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.
53. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.
54. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.
55. Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?
56. Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.
57. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
58. Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.