1 Kor. 15:21-38 Swahili Union Version (SUV)

21. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.

22. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.

23. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.

24. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.

25. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.

26. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.

27. Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo.

28. Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.

29. Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?

30. Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa?

31. Naam, ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, ninakufa kila siku.

32. Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nalipigana na hayawani wakali kule Efeso, nina faida gani? Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa.

33. Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.

34. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.

35. Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?

36. Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa;

37. nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo;

38. lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake.

1 Kor. 15