5. kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katika yeye, katika maneno yote, na maarifa yote;
6. kama ushuhuda wa Kristo ulivyothibitika kwenu;
7. hata hamkupungukiwa na karama yo yote, mkikutazamia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;
8. ambaye atawathibitisha hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.
9. Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.
10. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.
11. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu.
12. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.
13. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?
14. Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu kwenu, ila Krispo na Gayo;
15. mtu asije akasema kwamba mlibatizwa kwa jina langu.
16. Tena naliwabatiza watu wa nyumbani mwa Stefana; zaidi ya hao, sijui kama nalimbatiza mtu ye yote mwingine.
17. Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika.
18. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.
19. Kwa kuwa imeandikwa,Nitaiharibu hekima yao wenye hekima,Na akili zao wenye akili nitazikataa.
20. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?
21. Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa.
22. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima;