1. Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu,
2. kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu.
3. Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
4. Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu;
5. kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katika yeye, katika maneno yote, na maarifa yote;
6. kama ushuhuda wa Kristo ulivyothibitika kwenu;
7. hata hamkupungukiwa na karama yo yote, mkikutazamia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;
8. ambaye atawathibitisha hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.
9. Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.
10. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.
11. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu.