11. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;
12. basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.
13. Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.
14. Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi.
15. Naye Sulemani akaamka, na kumbe! Ni ndoto. Akaenda Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la BWANA, akatoa sadaka za kuteketezwa, akatoa na sadaka za amani; akawafanyia karamu watumishi wake wote.
16. Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake.
17. Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.
18. Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.
19. Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia.