1 Fal. 2:4-13 Swahili Union Version (SUV)

4. ili BWANA afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.

5. Na zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake.

6. Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia Ahera kwa amani.

7. Lakini uwafanyie mema wana wa Barzilai Mgileadi, wawe miongoni mwao walao mezani pako; kwa jinsi walivyonijilia nilipokuwa nimekimbia mbele ya Absalomu, ndugu yako.

8. Hata, angalia, yuko pamoja nawe Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu, ndiye aliyenilaani kwa laana kuu siku ile nilipokwenda Mahanaimu; lakini akashuka kunilaki kule Yordani, nami nikamwapia kwa BWANA, nikamwambia, Mimi sitakuua kwa upanga.

9. Basi kwa hiyo usimwachilie, kwa kuwa wewe u mtu wa akili; nawe utajua ikupasayo umtendee, na mvi zake utazishusha Ahera pamoja na damu.

10. Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi.

11. Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.

12. Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana.

13. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani?

1 Fal. 2