Zaburi 37:8-26 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu;usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya.

9. Watu watendao mabaya wataangamizwa,bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi.

10. Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka;utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona.

11. Lakini wapole wataimiliki nchi,hao watafurahia wingi wa fanaka.

12. Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu,na kumsagia meno kwa chuki.

13. Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu,kwani ajua mwisho wake u karibu.

14. Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao,wapate kuwaua maskini na fukara;wawachinje watu waishio kwa unyofu.

15. Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe,na pinde zao zitavunjwavunjwa.

16. Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifukuliko utajiri wa watu waovu wengi.

17. Maana nguvu za waovu zitavunjwa,lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu.

18. Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu,na urithi wao utadumu milele.

19. Hawataaibika zikifika nyakati mbaya;siku za njaa watakuwa na chakula tele.

20. Lakini waovu wataangamia,maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani;naam, watatoweka kama moshi.

21. Mtu mwovu hukopa bila kurudisha;lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu.

22. Waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi,lakini waliolaaniwa naye watafutiliwa mbali.

23. Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu,humlinda yule ampendezaye.

24. Ajapoanguka, haanguki akabaki chini,kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza.

25. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee;kamwe sijaona mwadilifu ameachwa na Mungu,au watoto wake wakiombaomba chakula.

26. Daima huwapa wengine kwa furaha na kukopesha,na watoto wake ni baraka.

Zaburi 37