Zaburi 31:2-18 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Unitegee sikio, uniokoe haraka!Uwe kwangu mwamba wa usalama,ngome imara ya kuniokoa.

3. Naam, wewe ni mwamba wangu na ngome yangu;kwa hisani yako uniongoze na kunielekeza.

4. Unitoe katika mtego walionitegea mafichoni;maana wewe ni kimbilio la usalama wangu.

5. Mikononi mwako naiweka roho yangu;umenikomboa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwaminifu.

6. Wawachukia wanaoabudu sanamu batili;lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu.

7. Nitashangilia na kufurahia fadhili zako,maana wewe waiona dhiki yangu,wajua na taabu ya nafsi yangu.

8. Wewe hukuniacha nitiwe mikononi mwa maadui zangu;umenisimamisha mahali pa usalama.

9. Unionee huruma, ee Mwenyezi-Mungu, niko taabuni;macho yangu yamechoka kwa huzuni,nimeishiwa nguvu mwilini na rohoni.

10. Maisha yangu yamekwisha kwa majonzi;naam, miaka yangu kwa kulalamika.Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika;hata mifupa yangu imekauka.

11. Nimekuwa dharau kwa maadui zangu wote;kioja kwa majirani zangu.Rafiki zangu waniona kuwa kitisho;wanionapo njiani hunikimbia.

12. Nimesahaulika kama mtu aliyekufa;nimekuwa kama chungu kilichovunjikavunjika.

13. Nasikia watu wakinongonezana,vitisho kila upande;wanakula njama dhidi yangu,wanafanya mipango ya kuniua.

14. Lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu.Nasema: “Wewe ni Mungu wangu!”

15. Maisha yangu yamo mikononi mwako;uniokoe na maadui zangu,niokoe na hao wanaonidhulumu.

16. Uniangalie kwa wema mimi mtumishi wako;uniokoe kwa fadhili zako.

17. Usiniache niaibike ee Mwenyezi-Mungu,maana mimi ninakuomba;lakini waache waovu waaibike,waache wapotelee kwa mshangao huko kuzimu.

18. Izibe midomo ya hao watu waongo,watu walio na kiburi na majivuno,ambao huwadharau watu waadilifu.

Zaburi 31