3. Lakini wakazi wa Gibeoni walipopata habari juu ya jinsi Yoshua alivyoitenda miji ya Yeriko na Ai,
4. waliamua kutumia hila. Wakatayarisha vyakula, wakapakiza magunia yaliyochakaa juu ya punda wao, viriba vilivyochakaa na kushonwa;
5. wakavaa viatu, nguo zilizochakaa na vyakula vyao vyote vilikuwa vikavu vilivyoota ukungu.
6. Basi, wakamwendea Yoshua kambini Gilgali, wakamwambia yeye na Waisraeli, “Sisi tumetoka nchi ya mbali; tafadhali tunaomba mfanye agano nasi.”
7. Lakini Waisraeli wakawajibu hao Wahivi, “Tunawezaje kufanya agano nanyi? Labda nyinyi mnaishi karibu nasi.”
8. Nao wakamwambia Yoshua, “Sisi tu watumishi wako.” Naye Yoshua akawauliza, “Nyinyi ni akina nani, na mnatoka wapi?”