Yoshua 7:5-13 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Watu wa Ai wakawaua Waisraeli thelathini na sita na kuwafukuza wengine kutoka lango la mji mpaka Shebarimu, wakawaua kwenye mteremko. Waisraeli wakafa moyo na kulegea kama maji.

6. Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao.

7. Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani!

8. Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao?

9. Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?”

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo?

11. Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao.

12. Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe.

13. Basi, inuka uwatakase watu, waambie wajitakase na kujitayarisha kwa siku ya kesho, maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: ‘Miongoni mwenu kuna vitu vilivyotolewa viangamizwe; hamwezi kuwakabili adui zenu mpaka vitu hivyo vimeondolewa kati yenu!

Yoshua 7