1. Baada ya kuishinda ile nchi, jumuiya yote ya Waisraeli ilikusanyika huko Shilo na kulisimika hema la mkutano.
2. Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ambayo hayakuwa yamegawiwa sehemu yao ya nchi.
3. Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni?
4. Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa.
5. Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini.